19 Aprili 2025 - 20:45
Source: Parstoday
Wayahudi wa Uingereza walaani vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza

Wawakilishi kadhaa wa jamiii ya Wayahudi nchini Uingereza wamelaani sera za serikali ya Benjamin Netanyahu, wakiishutumu kwa kutenda kinyume na "maadili ya Kiyahudi" kuhusiana na vita dhidi ya watu wa Gaza huko Palestina.

Sambamba na hayo, shirika la Marekani la Jewish Voice for Peace limetoa wito kwa utawala wa Rais Donald Trump kukomesha mara moja ufadhili kwa jeshi la Israel.

Katika barua ya wazi iliyochapishwa na Financial Times, wajumbe 36 wa Baraza la Wawakilishi wa Wayahudi wa Uingereza, chombo kikubwa zaidi kinachowakilisha jamii ya Wayahudi nchini Uingereza, wameandika kwamba "kinachotokea hakiwezi kuvumilika" na kwamba hawawezi tena kukaa kimya. "Maadili yetu ya Kiyahudi yanatulazimisha kusimama na kusema wazi."

Barua hiyo imesema, "Sera na hatua za serikali ya Netanyahu zinakinzana na maadili yetu ya Kiyahudi. Tunapinga vita. Tunahuzunishwa na kupoteza maisha Wapalestina."

Wawakilishi wa jamii ya Wayahudi nchini Uingereza pia wamelaani kuanzishwa tena mashambulizi ya Israel huko Gaza mnamo Machi 18 baada ya kusitisha mapigano kwa miezi miwili. 

Hii ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita vya Benjamin Netanyahu dhidi ya Gaza ambapo wajumbe wa baraza hilo wanaikosoa hadharani serikali ya Israel.

Katika muktadha huo, shirika la Jewish Voice for Peace limetoa wito kwa utawala wa Marekani kukomesha mara moja ufadhili kwa jeshi la Israel.

Taarifa ya shirika hilo imesema: "Serikali ya Marekani imewezesha mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza kwa kutuma silaha na makombora kwa Israel, na kusababisha vifo vya raia zaidi ya 60,000 wa ukanda huo."

Wayahudi wa Uingereza walaani vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, ulimwengu umeshuhudia jinsi jeshi la Israel lilivyowachoma kikatili Wapalestina 12 wakiwa hai katika mahema ya Mawasi, kwa kutumia mabomu ya Marekani.

Shirika hilo limezibebesha serikali za Israel na Marekani dhima ya kuwatesa kwa njaa watu wa Ukanda wa Gaza. 

Jewish Voice for Peace (JVP), yenye makao yake makuu mjini Berkeley, California, ni harakati ya Kiyahudi ya Marekani ambayo inalenga kuandaa vuguvugu la umma, kwa ushirikiano na Wapalestina na mashirika mengine yanayopinga ubeberu na yanayounga mkono ukombozi, ili kupambana na Uzayuni, kukabiliana na vitendo vya ukandamizaji vya utawala uvamizi wa Israel na kuhakikisha "kunapatikana haki, uhuru na usawa kwa Wapalestina pamoja na Mayahudi."

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha